13 Yehoashi akalala na babaze; na Yeroboamu akakaa katika kiti chake cha enzi; naye Yehoashi akazikwa huko Samaria, pamoja na wafalme wa Israeli.
14 Basi Elisha alikuwa ameshikwa na ugonjwa wake uliomwua; naye Yehoashi mfalme wa Israeli akatelemka amtazame, akamlilia mbele yake, akasema, Baba yangu! Baba yangu! Gari la Israeli na wapanda farasi wake!
15 Elisha akamwambia, Twaa uta na mishale; naye akatwaa uta na mishale.
16 Akamwambia mfalme wa Israeli, Weka mkono wako katika uta; naye akaweka mkono wake juu yake. Elisha akaweka mikono yake juu ya mikono ya mfalme.
17 Akasema, Lifungue dirisha linaloelekea mashariki; akalifungua. Basi Elisha akasema, Piga; akapiga. Akasema, Mshale wa BWANA wa kushinda, naam, mshale wa kushinda Shamu, kwa maana utawapiga Washami katika Afeki hata utakapowaangamiza.
18 Akasema, Itwae mishale; akaitwaa. Akamwambia mfalme wa Israeli, Piga chini; akaipiga nchi mara tatu, akaacha.
19 Yule mtu wa Mungu akamkasirikia, akasema, Ingalikupasa kupiga mara tano au mara sita; ndipo ungaliipiga Shamu hata kuiangamiza; bali sasa utaipiga Shamu mara tatu tu.