5 (BWANA akawapa Israeli mwokozi, nao wakatoka mikononi mwa Washami; wana wa Israeli wakakaa hemani mwao kama zamani za kwanza.
6 Lakini hawakuyaacha makosa ya nyumba ya Yeroboamu, ambayo kwa hayo aliwakosesha Israeli, lakini wakaendelea katika hayo; nayo ile Ashera ikakaa vivyo katika Samaria).
7 Kwa kuwa hakumwachia Yehoahazi watu ila wapandao farasi hamsini, na magari kumi, na askari elfu kumi waendao kwa miguu; kwa kuwa mfalme wa Shamu aliwaharibu, akawaponda mfano wa mavumbi yaliyokanyagwa.
8 Basi mambo yote ya Yehoahazi yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, na ushujaa wake, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli?
9 Yehoahazi akalala na babaze; wakamzika katika Samaria. Na Yehoashi mwanawe akatawala mahali pake.
10 Katika mwaka wa thelathini na saba wa Yoashi mfalme wa Yuda, Yehoashi mwana wa Yehoahazi alianza kutawala juu ya Israeli katika Samaria, akatawala miaka kumi na sita.
11 Akafanya yaliyo maovu machoni pa BWANA; hakuyaacha makosa ya Yeroboamu mwana wa Nebati, ambayo kwa hayo aliwakosesha Israeli; lakini akaendelea katika hayo.