6 ila hakuwaua watoto wa hao wauaji; kama ilivyoandikwa katika kitabu cha torati ya Musa, kama alivyoamuru BWANA, akisema, Mababa wasife kwa makosa ya wana, wala wana wasife kwa makosa ya mababa; lakini kila mtu atakufa kwa kosa lake mwenyewe.
7 Akawaua Waedomi katika Bonde la Chumvi watu elfu kumi; akautwaa Sela vitani, akauita jina lake Yoktheeli hata leo.
8 Ndipo Amazia akatuma wajumbe kwa Yehoashi mwana wa Yehoahazi mwana wa Yehu, mfalme wa Israeli, akisema, Njoo, tutazamane uso kwa uso.
9 Naye Yehoashi mfalme wa Israeli akatuma kwa Amazia mfalme wa Yuda, akisema, Mbaruti uliokuwako Lebanoni ulituma kwa mwerezi uliokuwako Lebanoni, kusema, Umwoze mwanangu binti yako; kukapita hayawani aliyekuwako Lebanoni, akaukanyaga ule mbaruti.
10 Kweli umepiga Edomu, na moyo wako umekutukuza; ujisifu basi, ukae nyumbani mwako. Mbona unataka kujitia bure katika madhara, hata uanguke, wewe na Yuda pamoja nawe?
11 Lakini Amazia hakutaka kusikia. Basi Yehoashi mfalme wa Israeli akakwea; wakatazamana uso kwa uso, yeye na Amazia mfalme wa Yuda, huko Beth-shemeshi ulio wa Yuda.
12 Yuda wakashindwa mbele ya Israeli; wakakimbia kila mtu hemani kwake.