29 Katika siku za Peka mfalme wa Israeli akaja Tiglath-pileseri mfalme wa Ashuru, akatwaa Iyoni, na Abel-beth-maaka, na Yanoa, na Kedeshi, na Hazori, na Gileadi, na Galilaya, nchi yote ya Naftali; akawahamisha hao watu mpaka Ashuru.
30 Na Hoshea mwana wa Ela akafanya fitina juu ya Peka mwana wa Remalia, akampiga, akamwua, akatawala mahali pake, katika mwaka wa ishirini wa Yothamu mwana wa Uzia.
31 Basi mambo yote ya Peka yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, tazama, yameandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli.
32 Katika mwaka wa pili wa Peka mwana wa Remalia mfalme wa Israeli Yothamu mwana wa Uzia mfalme wa Yuda alianza kutawala.
33 Alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala; akatawala miaka kumi na sita katika Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa Yerusha binti Sadoki.
34 Akafanya yaliyo mema machoni pa BWANA; akafanya kama yote aliyoyafanya Uzia baba yake.
35 Ila mahali pa juu hapakuondolewa; watu walikuwa wakitoa sadaka na kufukiza uvumba katika mahali pa juu. Ndiye aliyelijenga lango la juu la nyumba ya BWANA.