29 Lakini pamoja na hayo watu wa kila taifa wakajifanyia miungu yao wenyewe, wakaiweka katika nyumba za mahali pa juu, walipopafanya Wasamaria, kila taifa katika miji yao walimokaa.
30 Watu wa Babeli wakafanya Sukoth-benothi kuwa mungu wao, watu wa Kutha wakafanya Nergali, watu wa Hamathi wakafanya Ashima,
31 Waavi wakafanya Nibhazi na Tartaki; nao Wasefarvi wakawaunguza wana wao katika moto kwa Adrameleki na Anameleki, miungu ya Sefarvaimu.
32 Basi hivyo wakamcha BWANA, nao wakijifanyia wengine wao kuwa makuhani wa mahali pa juu, ambao waliwafanyia dhabihu katika nyumba za mahali pa juu.
33 Wakamcha BWANA, na kuitumikia miungu yao wenyewe, sawasawa na kawaida za mataifa ambao wao walihamishwa kutoka kwao.
34 Hata siku hii ya leo hufanya sawasawa na kawaida za kwanza; wala hawamwogopi BWANA, wala hawazifuati sheria zao, wala hukumu zao, wala ile torati, wala ile amri BWANA aliyowaamuru wana wa Yakobo, ambaye alimpa jina la Israeli;
35 hao ambao BWANA alifanya agano nao, akawaamuru, akasema, Msiche miungu mingine, wala kuisujudia, wala kuitumikia, wala kuitolea sadaka;