11 Mfalme wa Ashuru akawahamisha Israeli mpaka Ashuru, akawaweka katika Hala, na katika Habori, karibu na mto wa Gozani, na katika miji ya Wamedi;
12 kwa sababu hawakuitii sauti ya BWANA, Mungu wao, bali waliyahalifu maagano yake, mambo yote ambayo Musa mtumishi wa BWANA aliwaamuru, wasikubali kuyasikiliza, wala kuyatenda.
13 Ikawa katika mwaka wa kumi na nne wa kumiliki kwake mfalme Hezekia, Senakeribu, mfalme wa Ashuru, akapanda ili kupigana na miji yote ya Yuda yenye boma, akaitwaa.
14 Basi Hezekia, mfalme wa Yuda, akapeleka wajumbe waende Lakishi kwa mfalme wa Ashuru, kusema, Nimekosa; uniache ukarudi kwako; cho chote utakachoweka juu yangu, nitakichukua. Mfalme wa Ashuru akamtoza Hezekia, mfalme wa Yuda, talanta za fedha mia tatu, na talanta za dhahabu thelathini.
15 Hezekia akampa fedha yote iliyoonekana katika nyumba ya BWANA, na katika hazina za nyumba ya mfalme.
16 Wakati huo Hezekia aliiondoa dhahabu iliyokuwa juu ya milango ya hekalu la BWANA, na juu ya nguzo, ambazo Hezekia, mfalme wa Yuda, alikuwa amezitia dhahabu, akampa mfalme wa Ashuru.
17 Mfalme wa Ashuru akawatuma jemadari wake, na mkuu wa matowashi, na amiri wake, toka Lakishi, kwa mfalme Hezekia huko Yerusalemu, pamoja na jeshi kubwa. Nao wakakwea wakafika Yerusalemu. Na walipokwisha kufika, wakaja wakasimama karibu na mfereji wa birika la juu, lililo katika njia kuu ya kuuendea uwanda wa dobi.