6 Isaya akawaambia, Mwambieni bwana wenu maneno haya; BWANA asema hivi, Usiyaogope maneno hayo uliyoyasikia, ambayo watumishi wa mfalme wa Ashuru wamenitukana.
7 Tazama, nitatia roho ya hofu ndani yake, naye atasikia kivumi, na kuirudia nchi yake mwenyewe; nami nitamwangusha kwa upanga katika nchi yake mwenyewe.
8 Basi yule amiri akarudi, akamkuta mfalme wa Ashuru, anapigana na Libna; maana alikuwa amesikia ya kwamba ameondoka, akaacha Lakishi.
9 Na aliposikia habari ya Tirhaka mfalme wa Kushi, ya kwamba, Tazama, ametoka ili kupigana nawe; alituma wajumbe kwa Hezekia mara ya pili, kusema,
10 Mwambieni Hezekia, mfalme wa Yuda, maneno haya, mkisema, Asikudanganye Mungu wako unayemtumaini, akisema, Yerusalemu hautatiwa katika mikono ya mfalme wa Ashuru.
11 Tazama, umesikia ni mambo gani wafalme wa Ashuru waliyozitenda nchi zote, kwa kuziangamiza kabisa; je! Utaokoka wewe?
12 Je! Miungu ya mataifa wale, ambao baba zangu waliwaangamiza, imewaokoa? Yaani, Gozani, na Harani, na Resefu, na wana wa Adini waliokuwa katika Telasari?