8 Hezekia akamwambia Isaya, Je! Kutakuwa na ishara gani ya kwamba BWANA ataniponya, nami siku ya tatu nitapanda nyumbani kwa BWANA.
9 Isaya akamwambia, Jambo hili litakuwa ishara kwako, itokayo kwa BWANA, ya kwamba BWANA atalifanya neno hilo alilolinena; je! Kivuli kiendelee madaraja kumi, au kirudi nyuma madaraja kumi?
10 Hezekia akajibu, Ni jambo jepesi kivuli kuendelea madaraja kumi; la, hicho kivuli na kirudi nyuma madaraja kumi.
11 Isaya nabii akamlilia BWANA; akakirudisha nyuma kile kivuli madaraja kumi, ambayo kilikuwa kimeshuka katika madaraja ya Ahazi.
12 Wakati huo Merodak-baladani mwana wa Baladani, Mfalme wa Babeli, alipeleka barua na zawadi kwa Hezekia; kwa maana alipata habari kwamba Hezekia ameugua.
13 Hezekia akawasikiliza, akawaonyesha nyumba yote yenye vitu vyake vya thamani, fedha, na dhahabu, na manukato, na marhamu ya thamani, na nyumba yenye silaha zake, na vitu vyote vilivyoonekana katika hazina zake. Wala hapakuwa na kitu asichowaonyesha Hezekia, katika nyumba yake, wala katika ufalme wake wote.
14 Ndipo Isaya nabii akamwendea mfalme Hezekia, akamwambia, Wasemaje watu hawa? Nao wametoka wapi kuja kwako? Hezekia akasema, Wametoka katika nchi iliyo mbali, yaani Babeli.