1 Manase alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili alipoanza kutawala; akatawala miaka hamsini na mitano katika Yerusalemu, na jina la mamaye aliitwa Hefziba.
2 Akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA, sawasawa na machukizo ya mataifa, aliowafukuza BWANA mbele ya wana wa Israeli.
3 Kwa maana akapajenga tena mahali pa juu alipopaharibu Hezekia baba yake; akamjengea Baali madhabahu, akafanya Ashera kama alivyofanya Ahabu mfalme wa Israeli. Akajiinama mbele ya jeshi lote la mbinguni na kulitumikia.
4 Akazijenga madhabahu ndani ya nyumba ya BWANA, napo ndipo alipopanena BWANA, Katika Yerusalemu nitaliweka jina langu.
5 Akajenga madhabahu kwa ajili ya jeshi lote la mbinguni katika behewa mbili za nyumba ya BWANA.
6 Akampitisha mwanawe motoni, akatazama bao, akafanya uganga, akajishughulisha na hao wenye pepo wa utambuzi, na wachawi; akafanya mabaya mengi machoni pa BWANA, hata kumkasirisha.