15 kwa sababu wametenda yaliyo mabaya machoni pangu, na kunikasirisha, tangu siku ile walipotoka baba zao katika Misri, hata leo hivi.
16 Na Manase akazimwaga damu zisizo na hatia, nyingi sana, hata alipokuwa ameijaza Yerusalemu tangu upande huu hata upande huu; zaidi ya kosa lake alilowakosesha Yuda, kutenda yaliyo mabaya machoni pa BWANA.
17 Basi mambo yote ya Manase yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, na kosa lake alilolikosa, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Yuda?
18 Manase akalala na babaze, akazikwa katika bustani ya nyumba yake mwenyewe, yaani, bustani ya Uza. Na Amoni mwanawe akatawala mahali pake.
19 Amoni alikuwa na umri wa miaka ishirini na miwili alipoanza kutawala; akatawala miaka miwili huko Yerusalemu; na jina la mama yake aliitwa Meshulemethi, binti Haruzi wa Yotba.
20 Akafanya yaliyo maovu machoni pa BWANA, kama Manase babaye alivyofanya.
21 Akaiendea njia yote aliyoiendea baba yake, akazitumikia sanamu alizozitumikia baba yake, akaziabudu.