2 Akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA, sawasawa na machukizo ya mataifa, aliowafukuza BWANA mbele ya wana wa Israeli.
3 Kwa maana akapajenga tena mahali pa juu alipopaharibu Hezekia baba yake; akamjengea Baali madhabahu, akafanya Ashera kama alivyofanya Ahabu mfalme wa Israeli. Akajiinama mbele ya jeshi lote la mbinguni na kulitumikia.
4 Akazijenga madhabahu ndani ya nyumba ya BWANA, napo ndipo alipopanena BWANA, Katika Yerusalemu nitaliweka jina langu.
5 Akajenga madhabahu kwa ajili ya jeshi lote la mbinguni katika behewa mbili za nyumba ya BWANA.
6 Akampitisha mwanawe motoni, akatazama bao, akafanya uganga, akajishughulisha na hao wenye pepo wa utambuzi, na wachawi; akafanya mabaya mengi machoni pa BWANA, hata kumkasirisha.
7 Akaiweka sanamu ya kuchongwa ya Ashera aliyoifanya ndani ya nyumba, ambayo BWANA alimwambia Daudi, na Sulemani mwanawe, Katika nyumba hii, na katika Yerusalemu, niliouchagua miongoni mwa kabila zote za Israeli, nitaliweka jina langu milele;
8 wala sitawapotosha Israeli miguu watoke katika nchi niliyowapa baba zao; wakiangalia tu na kufanya sawasawa na yote niliyowaamuru, na kwa kuishika torati yote aliyowaamuru mtumishi wangu Musa.