13 Enendeni, mkamwulize BWANA kwa ajili yangu, na kwa ajili ya watu hawa, na kwa ajili ya Yuda yote, katika habari za maneno ya kitabu hiki kilichoonekana; kwa kuwa hasira ya BWANA ni kubwa aliyotukasirikia, kwa sababu baba zetu hawakuyaangalia maneno ya kitabu hiki, kufanya kama hayo yote tuliyoandikiwa.
14 Basi Hilkia kuhani, na Ahikamu, na Akbori, na Shafani, na Asaya, wakamwendea Hulda, nabii mke, mkewe Shalumu, mwana wa Tikva, mwana wa Harhasi, mtunza mavazi ya mfalme; (naye alikaa Yerusalemu katika mtaa wa pili;) wakasema naye.
15 Akawaambia, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi; Mwambieni mtu yule aliyewatuma ninyi kwangu,
16 BWANA asema hivi, Tazama, mimi nitaleta uovu juu ya mahali hapa, na juu yao wakaao hapa, naam, maneno yote ya kitabu alichokisoma mfalme wa Yuda;
17 kwa sababu wameniacha mimi, wameifukizia uvumba miungu mingine, ili wapate kunikasirisha kwa kazi yote ya mikono yao; kwa hiyo hasira yangu itawaka juu ya mahali hapa, isizimike.
18 Lakini yule mfalme wa Yuda, aliyewatuma ninyi kumwuliza BWANA, mtamwambia hivi, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kwa habari ya maneno yale uliyoyasikia,
19 kwa kuwa moyo wako ulikuwa mwororo, nawe ukajinyenyekesha mbele za BWANA, hapo ulipoyasikia maneno niliyoyanena juu ya mahali hapa, na juu ya wenyeji wake, ya kwamba watakuwa ukiwa na laana, nawe ulizirarua nguo zako, ukalia mbele zangu; basi, mimi nami nimekusikia wewe, asema BWANA.