8 Ikawa, Elisha, yule mtu wa Mungu, aliposikia kwamba mfalme wa Israeli ameyararua mavazi yake, ndipo akatuma mtu kwa mfalme, akisema, Mbona umeyararua mavazi yako? Na aje sasa kwangu mimi, naye atajua ya kuwa yuko nabii katika Israeli.
9 Basi Naamani akaja na farasi wake na magari yake, akasimama mlangoni pa nyumba ya Elisha.
10 Naye Elisha akampelekea mjumbe, akisema, Enenda ukaoge katika Yordani mara saba, na nyama ya mwili wako itakurudia, nawe utakuwa safi.
11 Lakini Naamani akakasirika, akaondoka, akasema, Tazama, nalidhania, Bila shaka atatoka kwangu, na kusimama, na kuomba kwa jina la BWANA, Mungu wake, na kupitisha mkono wake mahali penye ugonjwa, na kuniponya mimi mwenye ukoma.
12 Je! Abana na Farpari, mito ya Dameski, si bora kuliko maji yote ya Israeli? Je! Siwezi kujiosha ndani yake, na kuwa safi? Akageuka, akaondoka kwa hasira.
13 Watumishi wake wakamkaribia, wakamwambia, wakasema, Baba yangu, kama yule nabii angalikuambia kutenda jambo kubwa, usingalilitenda? Je! Si zaidi basi, akikuambia, Jioshe, uwe safi?
14 Ndipo akashuka, akajichovya mara saba katika Yordani, sawasawa na neno lake yule mtu wa Mungu; nayo nyama ya mwili wake ikarudi ikawa kama nyama ya mwili wa mtoto mchanga, akawa safi.