5 Naye alipofika, tazama, majemadari wa jeshi walikuwa wamekaa; naye akasema, Nimetumwa na neno kwako, Ee jemadari; Yehu akasema, Kwa yupi miongoni mwetu sote? Akasema, Kwako wewe, Ee jemadari.
6 Akainuka akaingia nyumbani; naye akayamimina yale mafuta kichwani mwake, akamwambia, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Nimekutia mafuta uwe mfalme juu ya watu wa BWANA, yaani, juu ya Israeli.
7 Nawe utawapiga nyumba ya Ahabu, bwana wako, ili nijilipize kisasi cha damu ya watumishi wangu manabii, na damu ya watumishi wote wa BWANA, mkononi mwa Yezebeli.
8 Kwa maana nyumba yote ya Ahabu wataangamia; nami nitamkatilia mbali kila mwanamume wa nyumba ya Ahabu, yeye aliyefungwa, na yeye asiyefungwa, katika Israeli.
9 Nami nitaifanya nyumba ya Ahabu kuwa kama nyumba ya Yeroboamu mwana wa Nebati, na kama nyumba ya Baasha mwana wa Ahiya.
10 Na mbwa watamla Yezebeli katika kiwanja cha Yezreeli, wala hapatakuwa na mtu wa kumzika. Akaufungua mlango, akakimbia.
11 Ndipo Yehu akatoka akawaendea watumishi wa bwana wake. Mmoja wao akamwuliza, Je! Ni amani? Huyu mwenye wazimu amekujia kwa nini? Akawaambia, Ninyi mnamjua mtu huyu na habari ya maneno yake.