8 Kwa maana nyumba yote ya Ahabu wataangamia; nami nitamkatilia mbali kila mwanamume wa nyumba ya Ahabu, yeye aliyefungwa, na yeye asiyefungwa, katika Israeli.
9 Nami nitaifanya nyumba ya Ahabu kuwa kama nyumba ya Yeroboamu mwana wa Nebati, na kama nyumba ya Baasha mwana wa Ahiya.
10 Na mbwa watamla Yezebeli katika kiwanja cha Yezreeli, wala hapatakuwa na mtu wa kumzika. Akaufungua mlango, akakimbia.
11 Ndipo Yehu akatoka akawaendea watumishi wa bwana wake. Mmoja wao akamwuliza, Je! Ni amani? Huyu mwenye wazimu amekujia kwa nini? Akawaambia, Ninyi mnamjua mtu huyu na habari ya maneno yake.
12 Wakasema, Ni uongo; haya, tuambie. Akasema, Aliniambia haya na haya, akisema, BWANA asema hivi, Nimekutia mafuta, uwe mfalme juu ya Israeli.
13 Basi wakafanya haraka, kila mtu akalitwaa vazi lake, na kulitia chini yake juu ya madaraja, wakapiga baragumu wakasema, Yehu ni mfalme.
14 Hivyo Yehu, mwana wa Yehoshafati, mwana wa Nimshi, akafanya fitina juu ya Yoramu.Basi Yoramu alikuwa akiulinda Ramoth-Gileadi, yeye na Israeli wote, kwa sababu ya Hazaeli mfalme wa Shamu.