1 Yehoshafati akalala na babaze, akazikwa pamoja na babaze katika mji wa Daudi; akatawala Yehoramu mwanawe mahali pake.
2 Naye alikuwa na ndugu, wana wa Yehoshafati, Azaria, na Yehieli, na Zekaria, na Azaria, na Mikaeli, na Shefatia; hao wote walikuwa wana wa Yehoshafati mfalme wa Israeli.
3 Baba yao akawapa zawadi kubwa, za fedha, na za dhahabu, na za tunu, pamoja na miji yenye maboma katika Yuda; lakini ufalme akampa Yehoramu, kwa sababu alikuwa mzaliwa wa kwanza.
4 Basi Yehoramu alipoinuliwa juu ya ufalme wa babaye, na kujitia nguvu, akawaua nduguze wote kwa upanga, na baadhi ya wakuu wa Israeli pia.