23 Akawaambia, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi; Mwambieni mtu huyo aliyewatuma kwangu,
24 BWANA asema hivi, Angalia, nitaleta mabaya juu ya mahali hapa, na juu ya wakaao, laana zote zilizoandikwa katika kitabu hicho walichokisoma mbele ya mfalme wa Yuda;
25 kwa sababu wameniacha mimi, na kuifukizia uvumba miungu mingine, ili wanikasirishe mimi kwa matendo yote ya mikono yao; kwa hiyo ghadhabu yangu imemwagika juu ya mahali hapa, wala isizimike.
26 Lakini mfalme wa Yuda, aliyewatuma kumwuliza BWANA, mtamwambia hivi, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi; Kwa habari ya maneno uliyoyasikia,
27 kwa kuwa moyo wako ulikuwa mwororo, nawe umejinyenyekeza mbele ya Mungu, uliposikia maneno yake juu ya mahali hapa, na juu ya wakaao, ukajinyenyekeza mbele zangu, na kuyararua mavazi yako, na kulia mbele zangu; mimi nami nimekusikia, asema BWANA.
28 Tazama, nitakukusanya kwa baba zako, nawe utawekwa kaburini mwako kwa amani, wala macho yako hayataona mabaya yote nitakayoyaleta juu ya mahali hapa, na juu ya wakaao. Basi wakamrudishia mfalme habari.
29 Ndipo mfalme akapeleka wajumbe, akawakusanya wazee wote wa Yuda na Yerusalemu.