10 Hivyo huduma ikatengenezwa, wakasimama makuhani mahali pao, na Walawi kwa zamu zao, kama alivyoamuru mfalme.
11 Wakachinja pasaka, nao makuhani wakamimina damu waliyopokea mikononi mwao, Walawi wakachuna.
12 Wakaziondoa sadaka za kuteketezwa, wawape wana wa watu, kama walivyogawanyika kufuata nyumba za mababa, ili wamtolee BWANA, kama ilivyoandikwa katika kitabu cha Musa. Nao ng’ombe wakawafanya vivyo hivyo.
13 Wakaioka moto pasaka kama ilivyo sheria; wakatokosa matoleo matakatifu vyunguni, na masufuriani, na makaangoni, wakawachukulia upesi wana wa watu wote.
14 Baadaye wakajiandalia wenyewe, na makuhani; kwa sababu makuhani, wana wa Haruni, walikuwa na kazi ya kutoa sadaka za kuteketezwa, na mafuta hata usiku; kwa hiyo Walawi wakajiandalia wenyewe, na makuhani, wana wa Haruni.
15 Nao waimbaji, wana wa Asafu wakasimama mahali pao, kama alivyoamuru Daudi, na Asafu, na Hemani, na Yeduthuni mwonaji wa mfalme; nao mabawabu walikuwa katika kila lango; hawakuhitaji kuondoka katika huduma yao, kwa kuwa ndugu zao Walawi wakawaandalia.
16 Basi huduma yote ya BWANA ikatengenezwa siku ile ile, kuifanya pasaka, na kutoa sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu ya BWANA, kama alivyoamuru mfalme Yosia.