18 Lakini Mungu je! Yamkini atakaa na watu duniani? Tazama, mbingu na mbingu za mbingu za mbingu hazikutoshi; siuze nyumba hii niliyoijenga!
19 Walakini umwangalie mtumwa wako anayoyaomba, na kusihi, Ee BWANA, Mungu wangu, usikie kilio na maombi anayoyaomba mtumwa wako mbele zako;
20 ili macho yako yafumbuke kwa nyumba hii mchana na usiku, mahali uliponena, ndipo utakapoliweka jina lako; usikie maombi atakayoomba mtumwa wako, akikabili mahali hapa.
21 Uyasikie atakayosihi mtumwa wako, na watu wako Israeli, watakapoomba wakikabili mahali hapa; naam, usikie toka makaoni mwako, toka mbinguni, nawe usikiapo, samehe.
22 Ikiwa mtu amemkosea mwenzake, akitiwa kiapo, aapishwe, naye akija na kuapa hapa mbele ya madhabahu yako nyumbani humu;
23 basi, usikie mbinguni, ukatende, ukawahukumu watumwa wako; ukimlipiza mwovu, kumpatilizia njia yake kichwani; ukamfanyie haki mwenye haki, ukimjalia kwa kadiri ya haki yake.
24 Ikiwa watu wako Israeli wamepigwa mbele ya adui zao, kwa sababu wamekukosa wewe; kama wakirejea kwako, na kulikiri jina lako, wakikuomba na kukusihi nyumbani humu;