25 basi usikie huko mbinguni, ukaisamehe dhambi ya watu wako Israeli, na kuwarejeza tena katika nchi uliyowapa wao na baba zao.
26 Ikiwa mbingu zimefungwa, hata hakuna mvua, kwa sababu wamekukosa wewe; kama wakiomba wakikabili mahali hapa, na kulikiri jina lako, na kuiacha dhambi yao, uwatesapo;
27 basi usikie huko mbinguni, ukaisamehe dhambi ya watumwa wako, na ya watu wako Israeli; uwafundishapo njia njema iwapasayo waiendee; ukainyeshee mvua nchi yako, uliyowapa watu wako iwe urithi.
28 Ikiwa nchi imeingia njaa, au tauni, au ukosefu wa mvua, au ukungu, au nzige, au panzi; ikiwa adui wamewahusuru katika nchi ya miji yao, au ukiwapo msiba wo wote, au uele wo wote;
29 yo yote atakayoyaomba na kusihi mtu awaye yote, au watu wako Israeli wote pamoja, watakaojua kila mtu pigo lake mwenyewe, na msiba wake mwenyewe, akiinyoshea mikono nyumba hii;
30 basi usikie huko mbinguni, ukaapo, ukasamehe, ukampatilize kila mtu kwa kadiri ya njia zake zote; wewe umjuaye moyo; (maana wewe peke yako ndiwe uijuaye mioyo ya wanadamu);
31 ili wakuche wewe, waziendee njia zako, siku zote watakazoishi katika nchi uliyowapa baba zetu.