26 Kisha huyo mlinzi akaona mtu mwingine anapiga mbio; mlinzi akamwita bawabu, akasema, Angalia, mtu mwingine anakuja mbio peke yake. Mfalme akasema, Huyu naye analeta habari.
27 Na huyo mlinzi akasema, Nionavyo mimi, kupiga mbio kwake yule wa kwanza ni kama kupiga mbio kwake Ahimaasi, mwana wa Sadoki. Naye mfalme akasema, Yeye ni mtu mwema, anakuja na habari njema.
28 Ahimaasi akainua sauti yake, akamwambia mfalme, Amani. Akainama mbele ya mfalme kifudifudi, akasema, Ahimidiwe BWANA, Mungu wako, aliyewatoa watu hao walioiinua mikono yao juu ya bwana wangu, mfalme.
29 Mfalme akauliza, Je! Yule kijana, Absalomu, yu salama? Ahimaasi akajibu, Yoabu aliponituma mimi mtumishi wa mfalme, mimi mtumishi wako, naliona kishindo kikubwa, lakini sikujua sababu yake.
30 Naye mfalme akasema, Geuka, usimame hapa. Akageuka, akasimama.
31 Na tazama, yule Mkushi akafika; Mkushi akasema, Nina habari kwa bwana wangu mfalme; kwa maana BWANA amekulipizia kisasi leo juu ya hao wote walioinuka kupigana nawe.
32 Naye mfalme akamwambia yule Mkushi, Yule kijana, Absalomu, je! Yu salama? Yule Mkushi akajibu, Adui za bwana wangu mfalme, na wote wainukao ili kukudhuru, na wawe kama alivyo yule kijana.