26 Samsoni akamwambia yule kijana aliyemshika mkono, Niache nizipapase nguzo ambazo nyumba hii inazikalia, nipate kuzitegemea.
27 Basi nyumba ile ilikuwa imejaa watu waume kwa wake; na wakuu wote wa Wafilisti walikuwamo humo, na juu ya dari palikuwa na watu elfu tatu waume kwa wake waliokuwa wakitazama, wakati Samsoni alipocheza.
28 Samsoni akamwita BWANA, akasema, Ee Bwana MUNGU, unikumbuke, nakuomba, ukanitie nguvu, nakuomba, mara hii tu, Ee Mungu, ili nipate kujilipiza kisasi juu ya Wafilisti kwa ajili ya macho yangu mawili.
29 Kisha Samsoni akazishika nguzo mbili za katikati ambazo nyumba ile ilikaa juu yake, akazitegemea, moja kwa mkono wake wa kuume na moja kwa mkono wake wa kushoto.
30 Samsoni akasema; Na nife pamoja na hawa Wafilisti. Akainama kwa nguvu zake zote; ile nyumba ikawaangukia hao wakuu, na watu wote waliokuwa ndani yake. Basi wale watu aliowaua wakati wa kufa kwake walikuwa wengi kuliko wale aliowaua wakati wa uhai wake.
31 Ndipo ndugu zake, na watu wote wa nyumba ya baba yake wakatelemka, wakamtwaa wakamchukua, wakamzika kati ya Sora na Eshtaoli, katika kiwanja cha kuzikia cha Manoa baba yake. Naye alikuwa mwamuzi wa Israeli muda wa miaka ishirini.