Isa. 64 SUV

1 Laiti ungepasua mbingu, na kushuka, ili milima iteteme mbele zako;

2 kama vile moto uchomapo vichaka, na moto uchemshapo maji; ili kuwajulisha adui zako jina lako, mataifa wakatetemeke mbele zako!

3 Ulipofanya mambo ya kutisha tusiyoyatazamia, ulishuka, milima ikatetema mbele zako.

4 Maana tangu zamani za kale watu hawakusikia, wala kufahamu kwa masikio, wala jicho halikuona Mungu, ila wewe, atendaye mambo kwa ajili yake amngojaye.

5 Wewe wamlaki yeye afurahiaye yaliyo haki na kuyatenda, watu wale wakukumbukao katika njia zako; tazama, ulikuwa na hasira, nasi tulitenda dhambi; tumekuwa katika mambo haya muda mwingi; nasi, je! Tutaokolewa?

6 Kwa maana sisi sote tumekuwa kama mtu aliye mchafu, na matendo yetu yote ya haki yamekuwa kama nguo iliyotiwa unajisi; sisi sote twanyauka kama jani, na maovu yetu yatuondoa, kama upepo uondoavyo.

7 Tena hapana aliitiaye jina lako, ajitahidiye akushike; kwa kuwa umetuficha uso wako, nawe umetukomesha kwa njia ya maovu yetu.

8 Lakini sasa, Ee BWANA, wewe u baba yetu; sisi tu udongo, nawe u mfinyanzi wetu; sisi sote tu kazi ya mikono yako.

9 Ee BWANA, usione hasira nyingi, wala usiukumbuke uovu siku zote; tazama, angalia, twakusihi, sisi sote tu watu wako.

10 Miji yako mitakatifu imekuwa jangwa, Sayuni umekuwa jangwa, Yerusalemu umekuwa ukiwa.

11 Nyumba yetu takatifu, nzuri, walimokusifu baba zetu, imeteketea moto; vitu vyetu vyote vyenye kupendeza vimeharibika.

12 Utajizuia usiyaangalie mambo haya, Ee BWANA? Utanyamaza, na kututesa sana?