Isa. 47 SUV

Kuaibishwa kwa Babeli

1 Haya, shuka, keti mavumbini,Ewe bikira, binti Babeli;Keti chini pasipo kiti cha enzi,Ewe binti wa Wakaldayo;Maana hutaitwa tena mwororo, mpenda anasa.

2 Twaa mawe ya kusagia, usage unga;Vua utaji wako, ondoa mavazi yako,Funua mguu wako, pita katika mito ya maji.

3 Uchi wako utafunuliwa,Naam, aibu yako itaonekana.Nitalipa kisasi; simkubali mtu ye yote.

4 Mkombozi wetu, BWANA wa majeshi ndilo jina lake,Mtakatifu wa Israeli.

5 Kaa kimya, ingia gizani,Ee binti wa Wakaldayo;Maana hutaitwa tena Malkia wa falme.

6 Nalikuwa nimekasirika na watu wangu, naliutia unajisi urithi wangu, nikawatia mkononi mwako; wewe hukuwatendea rehema; uliwatia wazee nira yako, nayo nzito sana.

7 Ukasema, Mimi nitakuwa bibi milele; hata hukuyatia hayo moyoni mwako, wala hukukumbuka mwisho wa mambo hayo.

8 Sasa, basi, sikia haya, wewe upendaye anasa, ukaaye na kujiona salama, wewe usemaye moyoni mwako, Mimi ndiye, wala hapana mwingine zaidi yangu mimi; sitaketi mfano wa mjane, wala sitajua kufiwa na watoto;

9 lakini mambo haya mawili yatakupata katika dakika moja siku moja, kufiwa na watoto, na ujane; yatakupata kiasi kitimilifu, uchawi wako ujapokuwa mwingi, na uganga wako mwingi mno.

10 Maana umeutumainia ubaya wako; umesema, Hapana anionaye; hekima yako, na maarifa yako yamekupotosha, nawe umesema moyoni mwako, Mimi ndiye, wala hapana mwingine zaidi yangu mimi.

11 Kwa sababu hiyo ubaya utakupata; wala hutajua kutopoa kwake; na msiba utakuangukia; hutaweza kuuondoa; na ukiwa utakupata kwa ghafula, usioujua.

12 Simama sasa na uganga wako, na wingi wa uchawi wako, uliojitaabisha nao tangu ujana wako; labda utaweza kupata faida, labda utaweza kushinda.

13 Umechoka kwa wingi wa mashauri yako; basi, na wasimame hao wajuao falaki, wazitazamao nyota, watabirio kila mwezi mambo ya mwezi huo, wakakuokoe na mambo yatakayokupata.

14 Tazama, watakuwa kama mabua makavu; moto utawateketeza; hawatajiokoa na nguvu za mwali wa moto; hautakuwa kaa la kukota moto, wala moto wa kukaa karibu nao.

15 Ndivyo yatakavyokuwa mambo hayo uliyojitaabisha nayo; wale waliofanya biashara nawe tangu ujana wako watatanga-tanga mbali nawe, kila mtu akienda zake; hapatakuwa na mtu wa kukuokoa.