Isa. 53 SUV

1 Ni nani aliyesadiki habari tuliyoileta?Na mkono wa BWANA amefunuliwa nani?

2 Maana alikua mbele zake kama mche mwororo,Na kama mzizi katika nchi kavu;Yeye hana umbo wala uzuri;Na tumwonapo hana uzuri hata tumtamani.

3 Alidharauliwa na kukataliwa na watu;Mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko;Na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao,Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu.

4 Hakika ameyachukua masikitiko yetu,Amejitwika huzuni zetu;Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa,Amepigwa na Mungu, na kuteswa.

5 Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu,Alichubuliwa kwa maovu yetu;Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake,Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.

6 Sisi sote kama kondoo tumepotea;Kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe;Na BWANA ameweka juu yakeMaovu yetu sisi sote.

7 Alionewa, lakini alinyenyekea,Wala hakufunua kinywa chake;Kama mwana-kondoo apelekwaye machinjoni,Na kama vile kondoo anyamazavyoMbele yao wakatao manyoya yake;Naam, hakufunua kinywa chake.

8 Kwa kuonewa na kuhukumiwa aliondolewa;Na maisha yake ni nani atakayeisimulia?Maana amekatiliwa mbali na nchi ya walio hai;Alipigwa kwa sababu ya makosa ya watu wangu.

9 Wakamfanyia kaburi pamoja na wabaya;Na pamoja na matajiri katika kufa kwake;Ingawa hakutenda jeuri,Wala hapakuwa na hila kinywani mwake.

10 Lakini BWANA aliridhika kumchubua;Amemhuzunisha;Utakapofanya nafsi yake kuwa dhabihu kwa dhambi,Ataona uzao wake, ataishi siku nyingi,Na mapenzi ya BWANA yatafanikiwa mkononi mwake;

11 Ataona mazao ya taabu ya nafsi yake, na kuridhika.Kwa maarifa yake mtumishi wangu mwenye hakiAtawafanya wengi kuwa wenye haki;Naye atayachukua maovu yao.

12 Kwa hiyo nitamgawia sehemu pamoja na wakuu,Naye atagawanya nyara pamoja nao walio hodari;Kwa sababu alimwaga nafsi yake hata kufa,Akahesabiwa pamoja na hao wakosao.Walakini alichukua dhambi za watu wengi,Na kuwaombea wakosaji.