Isa. 33 SUV

Unabii wa Kukombolewa kutoka kwa Watesi

1 Ole wako uharibuye ila hukuharibiwa, utendaye hila wala hukutendwa hila! Utakapokwisha kuharibu, utaharibiwa wewe; na utakapokwisha kutenda kwa hila, wao watakutenda hila wewe.

2 Ee BWANA, uturehemu; tumekungoja wewe; uwe wewe mkono wetu kila asububi, na wokovu wetu pia wakati wa taabu.

3 Kabila za watu wamekimbia wakisikia kelele za fujo; mataifa wametawanyika ulipojiinua nafsi yako.

4 Na mateka yako yatakumbwa kama wadudu wakumbavyo, wataruka juu yake kama arukavyo nzige.

5 BWANA ametukuka; kwa maana anakaa juu; amejaza Sayuni hukumu na haki.

6 Nyakati zako zitakuwa nyakati za kukaa imara; za wokovu tele na hekima na maarifa; kumcha BWANA ni hazina yake ya akiba.

7 Angalia, mashujaa wao wanalia nje, wajumbe wa amani wanalia kwa uchungu.

8 Njia kuu zimeachwa, msafiri amekoma; ameyavunja maagano, ameidharau miji, hamjali mtu.

9 Nchi inaomboleza, na kulegea; Lebanoni imetahayarika na kunyauka; Sharoni imekuwa kama jangwa; Bashani na Karmeli zimepukutika majani.

10 Basi, sasa nitasimama; asema BWANA; sasa nitajiinua, sasa nitajitukuza.

11 Ninyi mtachukua mimba ya makapi, mtazaa majani makavu; pumzi yenu ni moto utakaowateketeza wenyewe.

12 Nao mataifa watakuwa kama kuchoma chokaa, kama miiba iliyokatika, iteketezwayo motoni.

13 Sikieni, ninyi mlio mbali, niliyoyatenda; na ninyi mlio karibu, kirini uweza wangu.

14 Wenye dhambi walio katika Sayuni wanaogopa; tetemeko limewashika wasiomcha Mungu; Ni nani kwetu sisi awezaye kukaa na moto ulao; ni nani kwetu sisi awezaye kukaa na moto uteketezao milele?

15 Ni yeye aendaye kwa haki, anenaye maneno ya adili; ni yeye anayedharau faida ipatikanayo kwa dhuluma; akung’utaye mikono yake asipokee rushwa; azibaye masikio yake asisikie habari za damu; afumbaye macho yake asitazame uovu.

16 Huyu ndiye atakayekaa juu; majabali ni ngome yake; atapewa chakula chake; maji yake hayatakoma.

Nchi ya Mfalme Mkuu

17 Macho yako yatamwona mfalme katika uzuri wake, yataona nchi iliyoenea sana.

18 Moyo wako utatafakari hofu ile; Yuko wapi yeye aliyehesabu? Yuko wapi yeye aliyeupima ushuru? Yuko wapi yeye aliyeihesabu minara?

19 Hutawaona watu wale wakali; watu wa maneno magumu usiyoweza kuyafahamu; wenye lugha ya kigeni usiyoweza kuelewa nayo.

20 Angalia Sayuni, mji wa sikukuu zetu; macho yako yatauona Yerusalemu umekuwa kao la raha; hema isiyotanga-tanga; vigingi vyake havitang’olewa, wala kamba zake hazitakatika.

21 Bali huko BWANA atakuwa pamoja nasi, mwenye adhama; mahali penye mito mipana na vijito, pasipopita mashua na makasia yake; wala hapana merikebu ya vita itakayopita hapo.

22 Kwa maana BWANA ndiye mwamuzi wetu; BWANA ndiye mfanya sheria wetu; BWANA ndiye mfalme wetu; ndiye atakayetuokoa.

23 Kamba zako zimelegea; hawakuweza kukaza sana shina la mlingoti wao; hawakuweza kulikunjua tanga; ndipo mapato ya mateka yaligawanywa, hata wachechemeao walipata mateka.

24 Wala hapana mwenyeji atakayesema, Mimi mgonjwa; watu wakaao humo watasamehewa uovu wao.