Isa. 62 SUV

Uthibitisho wa Wokovu wa Sayuni

1 Kwa ajili ya Sayuni sitanyamaza, na kwa ajili ya Yerusalemu sitatulia, hata haki yake itakapotokea kama mwangaza, na wokovu wake kama taa iwakayo.

2 Na mataifa wataiona haki yako, na wafalme wote watauona utukufu wako; nawe utaitwa jina jipya, litakalotajwa na kinywa cha BWANA.

3 Nawe utakuwa taji ya uzuri katika mkono wa BWANA, na kilemba cha kifalme mkononi mwa Mungu wako.

4 Hutaitwa tena Aliyeachwa, wala nchi yako haitaitwa tena, Ukiwa; bali utaitwa Hefsiba; na nchi yako Beula; kwa kuwa BWANA anakufurahia, na nchi yako itaolewa.

5 Maana kama vile kijana amwoavyo mwanamwali, ndivyo wana wako watakavyokuoa wewe; na kama vile bwana arusi amfurahiavyo bibi arusi, ndivyo Mungu wako atakavyokufurahia wewe.

6 Nimeweka walinzi juu ya kuta zako, Ee Yerusalemu; hawatanyamaza mchana wala usiku; ninyi wenye kumkumbusha BWANA, msiwe na kimya;

7 wala msimwache akae kimya, mpaka atakapoufanya imara Yerusalemu, na kuufanya kuwa sifa duniani.

8 BWANA ameapa kwa mkono wake wa kuume, na kwa mkono wa nguvu zake, Hakika sitawapa adui zako nafaka yako tena kuwa chakula chao; wala wageni hawatakunywa divai yako, uliyoifanyia kazi.

9 Lakini walioivuna, ndio watakaoila, na kumhimidi BWANA; na walioichuma, ndio watakaoinywa, ndani ya nyua za patakatifu pangu.

10 Piteni, piteni, katika malango;Itengenezeni njia ya watu;Tutieni, tutieni barabara; toeni mawe yake;Twekeni bendera kwa ajili ya kabila za watu.

11 Tazama, BWANA ametangaza habari mpaka mwisho wa dunia,Mwambieni binti Sayuni,Tazama, wokovu wako unakuja;Tazama, thawabu yake i pamoja naye,Na malipo yake yako mbele zake.

12 Nao watawaita, Watu watakatifu,Waliokombolewa na BWANA;Nawe utaitwa, Aliyetafutwa,Mji usioachwa.