2 Nawe umchinjie pasaka BWANA, Mungu wako, katika kundi la kondoo na la ng’ombe, mahali atakapochagua BWANA apakalishe jina lake.
3 Usimle pamoja na mikate iliyotiwa chachu; siku saba utakula naye mikate isiyotiwa chachu, nayo ni mikate ya mateso; kwa maana ulitoka nchi ya Misri kwa haraka; ili upate kukumbuka siku uliyotoka nchi ya Misri, siku zote za maisha yako.
4 Wala isionekane kwako chachu muda wa siku saba katika mipaka yako yote; wala katika hiyo nyama uchinjayo siku ya kwanza jioni, kisilale cho chote usiku kucha hata asubuhi.
5 Usimchinje pasaka ndani ya malango yako yote akupayo BWANA, Mungu wako;
6 ila mahali atakapochagua BWANA, Mungu wako, apakalishe jina lake, ndipo mtakapomchinja pasaka jioni, katika machweo ya jua, kwa wakati kama uliotoka Misri.
7 Nawe umwoke na kumla mahali atakapochagua BWANA, Mungu wako; kisha asubuhi yake ugeuke uende hemani mwako.
8 Siku sita utakula mikate isiyotiwa chachu; na siku ya saba na uwe mkutano mtukufu kwa BWANA, Mungu wako, usifanye kazi yo yote.