13 nawe sema mbele ya BWANA, Mungu wako, Vitu vilivyo vitakatifu nimeviondoa katika nyumba yangu, nami mimewapa Mlawi, na mgeni, na yatima, na mjane, kwa mfano wa maagizo yako uliyoniusia yote; sikukosa maagizo yako yo yote, wala sikuyasahau;
14 katika vitu hivyo sikula wakati wa kukaa matanga mimi, wala sikuviondoa nikiwa na unajisi, wala sikutoa kwa ajili ya wafu katika vitu hivyo; sauti ya BWANA, Mungu wangu, nimeisikiza, nimefanya yote, kama ulivyoniamuru.
15 Uangalie kutoka makazi yako matakatifu mbinguni, uwabarikie watu wako Israeli, na nchi uliyotupa kama ulivyowaapia baba zetu, nchi imiminikayo maziwa na asali.
16 Leo hivi akuamuru BWANA, Mungu wako, kuzifanya amri hizi na hukumu; basi uzishike na kuzifanya kwa moyo wako wote na roho yako yote.
17 Umemwungama BWANA leo, kuwa ndiye Mungu wako, na kuwa yakupasa kutembea katika njia zake, na kushika amri zake na maagizo yake, na hukumu zake, na kusikiza sauti yake;
18 naye BWANA amekuungama hivi leo kuwa taifa iliyotengwa iwe yake yeye, kama alivyokuahidi, na kuwa yakupasa kushika maagizo yake yote;
19 na kuwa atakutukuza juu ya mataifa yote aliyoyafanya, kwa sifa, na jina, na heshima, nawe upate kuwa taifa takatifu kwa BWANA, Mungu wako, kama alivyosema.