8 Tena mlimkasirisha BWANA katika Horebu, BWANA akakasirika nanyi hata akataka kuwaangamiza.
9 Na hapo nilipokwea mlimani kwenda kuzipokea mbao za mawe, nazo ni mbao za agano BWANA alilofanya nanyi, ndipo nikakaa mle mlimani siku arobaini usiku na mchana; sikula chakula wala kunywa maji.
10 BWANA akanipa zile mbao mbili za mawe zimeandikwa kwa kidole cha Mungu; na juu yake yameandikwa maneno mfano wa yote aliyosema nanyi BWANA mle mlimani toka kati ya moto siku ya mkutano.
11 Ikawa mwisho wa siku arobaini usiku na mchana, BWANA alinipa zile mbao mbili za mawe, nazo ni mbao za agano.
12 BWANA akaniambia, Ondoka huko, shuka upesi; kwa kuwa watu wako uliowatoa Misri wamejiharibu; wamekengeuka mara katika njia niliyowaamuru; wamejifanyia sanamu ya kusubu.
13 Tena BWANA akasema nami zaidi, akaniambia, Nimeliona taifa hili; na tazama, ni taifa lenye shingo ngumu;
14 niache, nipate kuwaangamiza, na kulifuta jina lao chini ya mbingu; nami nitakufanya wewe uwe taifa kubwa lenye nguvu kuwapita wao.