15 Akawaambia watu; Mwe tayari siku ya tatu; msimkaribie mwanamke.
16 Ikawa siku ya tatu, wakati wa asubuhi, palikuwa na ngurumo na umeme, na wingu zito juu ya mlima, na sauti ya baragumu iliyolia sana. Watu wote waliokuwa kituoni wakatetemeka.
17 Musa akawatoa hao watu katika kituo, akawaleta ili waonane na Mungu; wakasimama pande za chini za kile kilima.
18 Mlima wa Sinai wote pia ukatoa moshi, kwa sababu BWANA alishuka katika moto; na ule moshi wake ukapanda juu kama moshi wa tanuu, mlima wote ukatetemeka sana.
19 Na hapo sauti ya baragumu ilipozidi kulia sana, Musa akanena, naye Mungu akamwitikia kwa sauti.
20 BWANA akaushukia mlima, juu ya kilele cha mlima; BWANA akamwita Musa aende hata kilele cha mlima; Musa akapanda juu.
21 Ndipo BWANA akamwambia Musa, Shuka chini, uwaonye watu wasije wakapasua njia waje kwa BWANA kutazama, kisha wengi miongoni mwao wakaangamia.