32 Tena kitu cho chote, wanyama hao mmojawapo atakachokiangukia, wakiisha kufa, kitakuwa ni najisi; kwamba ni chombo cha mti, au nguo, au ngozi, au gunia, chombo cho chote kitakachoangukiwa, ambacho ni chombo cha kufanyia kazi yo yote, lazima kitiwe ndani ya maji, nacho kitakuwa ni najisi hata jioni; ndipo kitakapokuwa ni safi.
33 Na kila chombo cha udongo, wanyama hao mmojawapo atakachokiangukia, kila kilichomo ndani yake kitakuwa ni najisi, na hicho chombo kitavunjwa.
34 Kila chakula kilichomo, ambacho ni kuliwa, hicho ambacho maji hutumiwa juu yake, kitakuwa ni najisi; na kila kinyweo ambacho ni cha kunywewa, kilichomo katika chombo kama hicho, kitakuwa ni najisi.
35 Na kila kitu kitakachoangukiwa na kipande cho chote cha mizoga yao kitakuwa najisi; kwamba ni tanuru, au meko ya vyungu, kitavunjwa vipande vipande; ni najisi vitu hivyo, navyo vitakuwa najisi kwenu.
36 Pamoja na hayo, chemchemi, au shimo, ambamo maji yakusanyika, vitakuwa ni safi; lakini hicho kitakachogusa mizoga yao kitakuwa ni najisi.
37 Na kipande cho chote cha mzoga kikiwa kimeangukia mbegu za kupandwa zitakazopandwa, zitakuwa safi.
38 Lakini kwamba hizo mbegu zilitiwa maji na cho chote cha mizoga yao kuziangukia, ni najisi kwenu.