29 Tena kwamba mtu anauza nyumba ya kukaa, iliyo ndani ya mji wenye kuta, ndipo ana ruhusa kuikomboa katika mwaka mmoja mzima baada ya kuiuza; atakuwa na amri ya kuikomboa muda wa mwaka mzima.
30 Na kama haikukombolewa katika muda wa mwaka mzima, ndipo hiyo nyumba iliyo ndani ya mji wenye kuta itathibitishwa milele kuwa ya huyo aliyeinunua, katika vizazi vyake; nayo haitatoka katika yubile.
31 Lakini nyumba za vijiji, ambavyo havikuzingirwa na kuta, zitahesabiwa pamoja na mashamba ya nchi; nazo zina ruhusa ya kukombolewa, nazo zitatoka katika yubile.
32 Pamoja na hayo, miji ya Walawi, nyumba za miji ya milki yao, Walawi wana ruhusa ya kuzikomboa majira yo yote.
33 Tena kama mtu mmoja wa hao Walawi akikomboa, ndipo nyumba iliyouzwa, na mji wa milki yake, itatoka katika yubile; maana, hizo nyumba za miji ya Walawi ni milki yao kati ya wana wa Israeli.
34 Lakini konde la malisho ya miji yao lisiuzwe kwa kuwa ni milki yao ya daima.
35 Na ikiwa ndugu yako amekuwa maskini, na mkono wake umelegea kwako, ndipo utamsaidia, atakaa nawe kama mgeni, na msafiri.