25 Kwani huyo mtu atakayekula mafuta ya mnyama, ambaye ni katika wanyama ambao watu husongeza sadaka kwa BWANA kwa moto, mtu huyo atakayekula mafuta hayo atakatiliwa mbali na watu wake.
26 Tena msiile damu yo yote, ama ya ndege, ama ya mnyama, katika nyumba zenu zote.
27 Mtu ye yote alaye damu, mtu huyo atakatiliwa mbali na watu wake.
28 BWANA akanena na Musa, na kumwambia,
29 Nena na wana wa Israeli uwaambie, Yeye asongezaye dhabihu yake ya sadaka za amani kwa BWANA, atamletea BWANA matoleo yake, kutoka katika ile dhabihu ya sadaka zake za amani;
30 mikono yake mwenyewe itamletea hizo sadaka za kusongezwa kwa moto; mafuta yake pamoja na kidari atayaleta, ili kwamba hicho kidari kitikiswe kuwa sadaka ya kutikiswa mbele ya BWANA.
31 Kuhani atayateketeza hayo mafuta juu ya madhabahu; lakini hicho kidari kitakuwa cha Haruni na cha wanawe.