10 Kisha Musa akatwaa hayo mafuta matakatifu ya kutia, akatia mafuta maskani, na vyote vilivyokuwamo, na kuvitakasa.
11 Kisha akanyunyiza hayo mafuta juu ya madhabahu mara saba, na kuitia mafuta madhabahu na vyombo vyake vyote, na birika na tako lake, ili kuvitakasa.
12 Kisha akamimina mafuta hayo ya kutia kichwani mwake Haruni, na kumtia mafuta, ili amtakase.
13 Kisha Musa akawaleta wana wa Haruni, na kuwavika kanzu, na kuwafunga mishipi, na kuwavika vilemba; kama BWANA alivyomwagiza Musa.
14 Kisha akamleta yule ng’ombe mume wa sadaka ya dhambi; na Haruni na wanawe wakaweka mikono yao katika kichwa cha huyo ng’ombe wa sadaka ya dhambi.
15 Kisha akamchinja; na Musa akaitwaa damu yake, akaitia katika pembe za madhabahu pande zote kwa kidole chake, akaitakasa madhabahu, kisha akaimwaga hiyo damu hapo chini ya madhabahu, na kuitakasa, ili afanye upatanisho kwa ajili yake.
16 Kisha akayatwaa mafuta yote yaliyokuwa katika matumbo yake, na kitambi kilichokuwa katika ini, na figo zake mbili, na mafuta yake, na Musa akayateketeza juu ya madhabahu.