22 Kisha akamsongeza kondoo mume wa pili, huyo kondoo wa kuwaweka wakfu; na Haruni na wanawe wakaweka mikono yao kichwani mwa huyo kondoo.
23 Kisha akamchinja; na Musa akatwaa katika damu yake, na kuitia katika ncha ya sikio la kuume la Haruni, na katika chanda chake cha gumba cha mkono wake wa kuume, na katika kidole cha gumba cha guu lake la kuume.
24 Kisha akawaleta wana wa Haruni, na Musa akaitia hiyo damu katika ncha za masikio ya kuume, na katika vyanda vya gumba vya mikono yao ya kuume, na katika vidole vya gumba vya maguu yao ya kuume; kisha Musa akainyunyiza hiyo damu katika madhabahu pande zote.
25 Kisha akayatwaa hayo mafuta, na mkia wenye mafuta, na mafuta yote yaliyokuwa katika matumbo, na kitambi cha ini, na figo mbili, na mafuta yake, na mguu wa nyuma wa upande wa kuume;
26 kisha katika kikapu cha mikate isiyotiwa chachu, kilichokuwa pale mbele za BWANA, akatwaa mkate mmoja usiochachwa, na mkate mmoja ulioandaliwa na mafuta na kaki moja nyembamba, akaiweka juu ya mafuta, na juu ya huo mguu wa nyuma wa upande wa kuume;
27 kisha akaweka vyote katika mikono ya Haruni, na katika mikono ya wanawe, na kuvitikisa huku na huku viwe sadaka ya kutikiswa mbele za BWANA.
28 Kisha Musa akavitwaa tena mikononi mwao, na kuviteketeza juu ya madhabahu, juu ya hiyo sadaka ya kuteketezwa vilikuwa vya kuwaweka wakfu, ni harufu nzuri; ilikuwa dhabihu iliyosongezwa kwa BWANA kwa moto.