12 Siku nyingi zikapita, akafa binti Shua, mkewe Yuda. Yuda akafarijika, akaenda kwa watu wake wawakatao manyoya kondoo huko Timna, yeye na mwenzake Hira, Mwadulami.
13 Huyo Tamari akapewa habari, kusema, Mkweo anakwenda Timna, akate manyoya ya kondoo zake.
14 Basi akavua nguo za ujane wake, akajivika utaji, akajifunika uso, akakaa mlangoni pa Enaimu, karibu na njia ya kuendea Timna. Maana aliona ya kwamba Shela amekuwa mtu mzima, wala hakuozwa awe mkewe.
15 Yuda alipomwona alimdhania kuwa ni kahaba, maana amejifunika uso.
16 Akamgeukia kando ya njia, akasema, Niruhusu niingie kwako. Maana hakujua ya kuwa ni mkwewe. Akamwuliza, Utanipa nini, ukiingia kwangu?
17 Akasema, Nitakuletea mwana-mbuzi wa kundini. Naye akamwuliza, Je! Utanipa rehani hata utakapomleta?
18 Akasema, Nikupe rehani gani? Akamjibu, Pete yako ya muhuri, na kamba yake, na fimbo yako iliyo mkononi mwako. Basi akampa, akaingia kwake, naye akapata mimba.