7 Bwana ameitupilia mbali madhabahu yake,Amepachukia patakatifu pake;Amezitia katika mikono ya hao aduiKuta za majumba yake;Wamepiga kelele ndani ya nyumba ya BWANAKama katika siku ya kusanyiko la makini.
8 BWANA amekusudia kuuharibuUkuta wa binti Sayuni;Ameinyosha hiyo kamba,Hakuuzuia mkono wake usiangamize;Bali amefanya boma na ukuta kuomboleza;Zote pamoja hudhoofika.
9 Malango yake yamezama katika nchi;Ameyaharibu makomeo yake na kuyavunja;Mfalme wake na wakuu wake wanakaaKati ya mataifa wasio na sheria;Naam, manabii wake hawapati maonoYatokayo kwa BWANA.
10 Wazee wa binti Sayuni huketi chini,Hunyamaza kimya;Wametupa mavumbi juu ya vichwa vyao,Wamejivika viunoni nguo za magunia;Wanawali wa Yerusalemu huinama vichwa vyaoKuielekea nchi.
11 Macho yangu yamechoka kwa machozi,Mtima wangu umetaabika;Ini langu linamiminwa juu ya nchiKwa uharibifu wa binti ya watu wangu;Kwa sababu watoto wachanga na wanyonyao,Huzimia katika mitaa ya mji.
12 Wao huwauliza mama zao,Zi wapi nafaka na divai?Hapo wazimiapo kama waliojeruhiwaKatika mitaa ya mji,Hapo walipomiminika nafsi zaoVifuani mwa mama zao.
13 Nikushuhudie nini? Nikufananishe na nini,Ee Binti Yerusalemu?Nikusawazishe na nini, nipate kukufariji,Ee bikira binti Sayuni?Kwa maana uvunjifu wako ni mkuu kama bahari,Ni nani awezaye kukuponya?