1 Wewe u mwenye haki, Ee BWANA, nitetapo nawe, lakini nitasema nawe katika habari ya haki. Mbona njia ya wabaya inasitawi? Mbona wote watendao hila wanakaa salama?
2 Umewapanda, naam, wametia mizizi, wanakua, naam, wanazaa matunda; katika vinywa vyao u karibu, bali katika mioyo yao u mbali.
3 Lakini wewe, BWANA, wanijua; umeniona, umeujaribu moyo wangu, jinsi unavyokuelekea; uwakokote kama kondoo waendao kuchinjwa, ukawaweke tayari kwa siku ya kuchinjwa.
4 Hata lini itaomboleza nchi, na kukauka majani ya nchi yote? Kwa ajili ya mabaya yao wakaao ndani yake, wanyama wameangamia na ndege pia; kwa sababu walisema, Hatauona mwisho wetu.
5 Ikiwa umepiga mbio pamoja na hao waendao kwa miguu, nao wamekuchosha, basi wawezaje kushindana na farasi? Na ujapokuwa katika nchi ya amani u salama, lakini utafanyaje hapo katika kiburi cha Yordani?
6 Kwa maana hata ndugu zako, na nyumba ya baba yako, wamekutenda mambo ya hila; naam, wamepiga kelele nyuma yako; usiwasadiki, wajapokuambia maneno mazuri.
7 Nimeiacha nyumba yangu, nimeutupa urithi wangu; nimemtia mpenzi wangu katika mikono ya adui zake.