12 Watekao nyara wamepanda juu ya vilele vya milima katika nyika; kwa maana upanga wa BWANA utakula toka upande mmoja wa nchi hata upande wa pili wa nchi; hapana mwenye mwili atakayekuwa na amani.
13 Wamepanda ngano, lakini watavuna miiba; wamejiumiza nafsi zao, lakini hawatakuwa na faida; naam, tahayarini kwa ajili ya matunda yenu, kwa sababu ya hasira kali ya BWANA.
14 BWANA asema hivi juu ya jirani zangu wote walio wabaya, waugusao urithi wangu niliowarithisha watu wangu Israeli, Tazama, nitawang’oa katika nchi yao, nami nitaing’oa nyumba ya Yuda isiwe kati yao.
15 Tena itakuwa, baada ya kuwang’oa, nitarudi na kuwahurumia; nami nitawaleta tena, kila mtu aingie katika urithi wake, na kila mtu aingie katika nchi yake.
16 Kisha itakuwa, ikiwa watajifunza kwa bidii njia za watu wangu, kuapa kwa jina langu, Kama BWANA aishivyo, vile vile kama walivyowafundisha watu wangu kuapa kwa Baali, ndipo watakapojengwa kati ya watu wangu.
17 Bali, kama hawataki kusikia, kung’oa nitaling’oa taifa lile, na kuliangamiza kabisa, asema BWANA.