1 BWANA akasema hivi, Enenda ukanunue gudulia la mfinyanzi, ukachukue pamoja nawe baadhi ya wazee wa watu, na baadhi ya wazee wa makuhani;
2 ukatoke uende mpaka bonde la mwana wa Hinomu lililo karibu na mahali pa kuingia kwa lango la vigae, ukahubiri huko maneno nitakayokuambia,
3 ukisema, Lisikieni neno la BWANA, enyi wafalme wa Yuda, na wenyeji wa Yerusalemu; BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli asema hivi, Angalieni, nitaleta mabaya juu ya mahali hapa, ambayo mtu ye yote akisikia habari yake, masikio yake yatawaka.
4 Kwa sababu wameniacha mimi, nao wamepafanya mahali hapa kuwa mahali pageni, nao hapa wamewafukizia uvumba miungu mingine wasiowajua, wala wao, wala baba zao, wala wafalme wa Yuda; nao wamepajaza mahali hapa damu ya wasio na hatia;
5 nao wamemjengea Baali mahali pake palipo juu, ili kuwachoma moto wana wao, wawe sadaka za kuteketezwa kwa Baali; tendo nisiloliamuru mimi, wala kulinena, wala halikuingia moyoni mwangu;
6 basi, angalieni, siku zinakuja, asema BWANA, ambazo katika siku hizo mahali hapa hapataitwa tena Tofethi, wala Bonde la mwana wa Hinomu, bali, Bonde la Machinjo.
7 Nami nitalitangua shauri la Yuda na Yerusalemu mahali hapa; nami nitawaangusha kwa upanga mbele za adui zao, na kwa mkono wa watu watafutao roho zao; na mizoga yao nitawapa ndege wa angani na wanyama wakali wa nchi, iwe chakula chao.