1 Basi Pashuri, mwana wa Imeri, kuhani, aliyekuwa msimamizi mkuu katika nyumba ya BWANA, alimsikia Yeremia alipokuwa akitabiri maneno hayo.
2 Ndipo Pashuri akampiga Yeremia, nabii, akamtia katika mkatale, uliokuwa pale penye lango la juu la Benyamini, lililokuwa katika nyumba ya BWANA.
3 Hata ikawa, asubuhi, Pashuri huyo akamtoa Yeremia katika mkatale. Ndipo Yeremia akamwambia, BWANA hakukuita jina lako Pashuri, bali Magor-misabibu.
4 Maana BWANA asema hivi, Tazama, nitakufanya kuwa hofu kuu kwa nafsi yako, na kwa rafiki zako wote; nao wataanguka kwa upanga wa adui zao, na macho yako yataona hayo; nami nitatia Yuda yote katika mikono ya mfalme wa Babeli, naye atawachukua mateka mpaka Babeli, na kuwaua kwa upanga.
5 Tena mali zote za mji huu, na mapato yake yote, na vitu vyake vya thamani vyote pia, naam, hazina zote za wafalme wa Yuda, nitavitia katika mikono ya adui zao, watakaowateka nyara, na kuwakamata, na kuwachukua mpaka Babeli.
6 Na wewe, Pashuri, na watu wote wanaokaa katika nyumba yako, mtakwenda utumwani; nawe utafika Babeli, na huko utakufa, na huko utazikwa, wewe, na rafiki zako wote, uliowatabiria maneno ya uongo.
7 Ee BWANA, umenihadaa, nami nimehadaika; wewe una nguvu kuliko mimi, ukashinda; nimekuwa kitu cha kuchekesha, mchana kutwa; kila mtu hunidhihaki.