1 BWANA akanionyesha, na tazama, vikapu viwili vya tini, vimewekwa mbele ya hekalu la BWANA, baada ya Nebukadreza, mfalme wa Babeli, kumchukua mateka Yekonia, mwana wa Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, na wakuu wa Yuda, pamoja na mafundi na wafua chuma, kutoka Yerusalemu, kuwaleta Babeli.
2 Kikapu kimoja kilikuwa na tini nzuri sana, kama tini zilizotangulia kuiva; na kikapu cha pili kilikuwa na tini mbovu sana zisizoweza kuliwa, kwa kuwa zilikuwa mbovu sana.
3 Ndipo BWANA akaniambia, Unaona nini Yeremia? Nikasema, Naona tini; tini nzuri zilizo nzuri sana; na tini mbovu zilizo mbovu sana, zisizoweza kuliwa, kwa kuwa ni mbovu sana.
4 Kisha neno la BWANA likanijia, kusema,
5 BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kama zilivyo tini hizi nzuri, ndivyo nitakavyowaangalia mateka wa Yuda, niliowatoa katika mahali hapa, waende mpaka nchi ya Wakaldayo, wapate mema.
6 Kwa maana nitawatulizia macho yangu, wapate mema, nami nitawaingiza katika nchi hii tena; nami nitawajenga, wala sitawabomoa; nitawapanda wala sitawang’oa.