1 Mwanzo wa kumiliki kwake Yehoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, neno hili lilitoka kwa BWANA, kusema,
2 BWANA asema hivi, Simama katika uwanja wa nyumba ya BWANA, useme na miji yote ya Yuda, wajao ili kuabudu katika nyumba ya BWANA; sema nao maneno yote ninayokuamuru kuwaambia, usizuie hata neno moja.
3 Labda watasikia, na kughairi na kuacha kila mtu njia yake mbaya; ili niyaghairi mabaya niliyokusudia kuwatenda, kwa sababu ya uovu wa matendo yao.
4 Nawe utawaambia, BWANA asema hivi, Kama hamtaki kunisikia, kwenda katika sheria yangu, niliyoiweka mbele yenu,
5 kuyasikiliza maneno ya watumishi wangu, manabii, ninaowatuma kwenu, naam, nikiondoka mapema na kuwatuma; lakini ninyi hamkuwasikiliza;
6 basi, nitafanya nyumba hii kuwa kama Shilo, na mji huu nitaufanya kuwa laana kwa taifa zote za dunia.