10 BWANA asema hivi, katika mahali hapo ambapo mnasema kwamba ni ukiwa, hapana mwanadamu wala mnyama, naam, katika miji ya Yuda na katika njia za Yerusalemu, zilizo ukiwa, hazina mwanadamu wala mwenyeji wala mnyama,
11 itasikilikana tena sauti ya furaha na sauti ya shangwe, sauti ya bwana arusi na sauti ya bibi arusi, sauti yao wasemao Mshukuruni BWANA wa majeshi, maana BWANA ni mwema, rehema zake ni za milele; na sauti zao waletao sadaka za shukrani nyumbani kwa BWANA. Kwa kuwa nitawarudisha wafungwa wa nchi hii kama kwanza, asema BWANA.
12 BWANA wa majeshi asema hivi, Katika mahali hapa, palipo ukiwa, hapana mwanadamu wala mnyama, na katika miji yake yote, yatakuwapo makao ya wachungaji wakizilaza kondoo zao.
13 Katika miji ya nchi ya vilima, katika miji ya nchi tambarare, katika miji ya Negebu, na katika nchi ya Benyamini, na katika mahali palipo karibu na Yerusalemu, na katika miji ya Yuda, makundi ya kondoo yatapita tena chini ya mikono yake awahesabuye, asema BWANA.
14 Tazama, siku zinakuja, asema BWANA, nitakapolitimiza neno lile jema nililolinena, katika habari za nyumba ya Israeli, na katika habari za nyumba ya Yuda.
15 Katika siku zile, na wakati ule, nitamchipushia Daudi Chipukizi la haki; naye atafanya hukumu na haki katika nchi hii.
16 Katika siku zile Yuda ataokolewa, na Yerusalemu utakaa salama, na jina lake atakaloitwa ni hili, BWANA ni haki yetu.