1 Neno hili ndilo lililomjia Yeremia, kutoka kwa BWANA, hapo Nebukadreza, mfalme wa Babeli, na jeshi lake lote, na falme zote za dunia zilizokuwa chini ya mamlaka yake, na kabila zote za watu, walipopigana na Yerusalemu, na miji yake yote, kusema,
2 BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Enenda ukaseme na Sedekia, mfalme wa Yuda, ukamwambie, BWANA asema hivi, Tazama, nitatia mji huu katika mikono ya mfalme wa Babeli, naye atauteketeza kwa moto;
3 tena wewe hutaokoka mkononi mwake, lakini utakamatwa kweli kweli, na kutiwa katika mikono yake; na macho yako yatayatazama macho ya mfalme wa Babeli, naye atasema nawe mdomo kwa mdomo, nawe utakwenda Babeli.
4 Hata hivyo lisikie neno la BWANA, Ee Sedekia, mfalme wa Yuda; BWANA asema hivi katika habari zako; hutakufa kwa upanga;
5 utakufa katika amani; na kwa mafukizo ya baba zako, wafalme wa zamani waliokutangulia, ndivyo watakavyokufukizia; nao watakulilia, Aa, BWANA! Kwa maana mimi nimelinena neno hili, asema BWANA.
6 Basi Yeremia, nabii, akamwambia Sedekia, mfalme wa Yuda, maneno hayo yote katika Yerusalemu,
7 wakati ule jeshi la Babeli walipopigana na Yerusalemu na miji yote ya Yuda iliyosalia, na Lakishi, na Azeka; kwa maana miji hiyo tu ndiyo iliyosalia katika miji ya Yuda yenye maboma.