4 Hata hivyo lisikie neno la BWANA, Ee Sedekia, mfalme wa Yuda; BWANA asema hivi katika habari zako; hutakufa kwa upanga;
5 utakufa katika amani; na kwa mafukizo ya baba zako, wafalme wa zamani waliokutangulia, ndivyo watakavyokufukizia; nao watakulilia, Aa, BWANA! Kwa maana mimi nimelinena neno hili, asema BWANA.
6 Basi Yeremia, nabii, akamwambia Sedekia, mfalme wa Yuda, maneno hayo yote katika Yerusalemu,
7 wakati ule jeshi la Babeli walipopigana na Yerusalemu na miji yote ya Yuda iliyosalia, na Lakishi, na Azeka; kwa maana miji hiyo tu ndiyo iliyosalia katika miji ya Yuda yenye maboma.
8 Neno hili ndilo lililomjia Yeremia, kutoka kwa BWANA, baada ya wakati ule mfalme Sedekia alipofanya agano na watu wote waliokuwa katika Yerusalemu, kuwatangazia habari ya uhuru;
9 ya kwamba kila mtu amweke huru mtumwa wake, na kila mtu amweke huru mjakazi wake, ikiwa yule mwanamume au yule mwanamke ni Mwebrania; mtu ye yote asiwatumikishe, yaani, asimtumikishe Myahudi, nduguye;
10 na wakuu wote, na watu wote, wakati, waliofanya agano hilo, ya kwamba kila mtu amweke huru mtumwa wake na mjakazi wake, mtu ye yote asiwatumikishe tena; wakatii, wakawaacha.