1 Neno lililomjia Yeremia, katika habari za Wayahudi wote waliokaa katika nchi ya Misri, waliokaa Migdoli, na Tahpanesi, na Nofu, na katika nchi ya Pathrosi, kusema,
2 BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Ninyi mmeona mabaya yote niliyoleta juu ya Yerusalemu, na juu ya miji yote ya Yuda; na, tazama, ni ukiwa leo, wala hapana mtu akaaye ndani yake;
3 kwa sababu ya uovu wao, waliotenda ili kunikasirisha, kwa kuwa walikwenda kufukiza uvumba, na kuwatumikia miungu mingine, ambao hawakuwajua, wao, wala ninyi, wala baba zenu.
4 Tena nalituma kwenu watumishi wangu wote, manabii, nikiamka mapema na kuwatuma, nikisema, Basi ninyi; msilifanye chukizo hili linichukizalo.