4 Tena nalituma kwenu watumishi wangu wote, manabii, nikiamka mapema na kuwatuma, nikisema, Basi ninyi; msilifanye chukizo hili linichukizalo.
5 Lakini hawakusikiliza, wala hawakutega masikio yao, ili wageuke na kuacha uovu wao, wasifukizie uvumba miungu mingine.
6 Kwa sababu hiyo ghadhabu yangu, na hasira yangu, zilimwagika, nazo ziliwaka katika miji ya Yuda, na katika njia kuu za Yerusalemu, na miji hiyo imeachwa ukiwa, na kuharibika, kama ilivyo leo.
7 Basi, sasa, BWANA, Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kwa nini mnafanya uovu huu mkubwa juu ya nafsi zenu wenyewe, kujikatilia mbali mwanamume na mwanamke, mtoto mchanga na anyonyaye, mtoke kati ya Yuda, msijiachie mtu abakiye;
8 kwa kuwa mnanikasirisha kwa matendo ya mikono yenu, mkifukizia uvumba miungu mingine katika nchi ya Misri, mlikokwenda kukaa ugenini; mpate kukatiliwa mbali, na kuwa laana, na aibu, katika mataifa yote ya dunia?
9 Je! Mmeusahau uovu wa baba zenu, na uovu wa wafalme wa Yuda, na uovu wa wake zao, na uovu wenu wenyewe, na uovu wa wake zenu, walioutenda katika nchi ya Yuda, na katika njia kuu za Yerusalemu?
10 Hawajanyenyekea hata leo, wala hawakuogopa, wala hawakuenenda katika sheria yangu, wala katika amri zangu, nilizoweka mbele yenu, na mbele ya baba zenu.