26 Njoni juu yake toka mpaka ulio mbali;Zifungueni ghala zake;Mfanyeni kuwa magofu na kumharibu kabisa;Msimsazie kitu cho chote.
27 Wachinjeni mafahali wake wote;Na watelemkie machinjoni;Ole wao! Maana siku yao imewadia,Wakati wa kujiliwa kwao.
28 Sauti yao wakimbiao na kuokoka,Kutoka katika nchi ya Babeli,Ili kutangaza Sayuni kisasi cha BWANA, Mungu wetu,Kisasi cha hekalu lake.
29 Waiteni wapiga mishale juu ya Babeli,Naam, wote waupindao upinde;Pangeni hema kumzunguka pande zote;Ili asiokoke hata mtu mmoja wao;Mlipeni kwa kadiri ya kazi yake;Mtendeni sawasawa na yote aliyoyatenda;Kwa sababu amefanya kiburi juu ya BWANA,Juu yake aliye Mtakatifu wa Israeli.
30 Kwa sababu hiyo vijana wake wataanguka katika njia kuu zake, na watu wake wa vita, wote pia, watanyamazishwa katika siku hiyo, asema BWANA.
31 Tazama, mimi ni juu yako, Ewe mwenye kiburi, asema Bwana, BWANA wa majeshi; maana siku yako imewadia, wakati nitakapokujilia.
32 Na mwenye kiburi atajikwaa, na kuanguka, wala hapana atakayemwinua; nami nitawasha moto katika miji yake, nao utawala wote wamzungukao pande zote.